Mishahara kupanda kimya kimya

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema hakuna lazima ya kutangaza nyongeza ya mishahara hadharani, kwani mshahara ni siri ya mtumishi na kwa kupandisha wazi kuna madhara yake. Waziri Mkuu alitoa ufafanuzi huo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo (Chadema) aliyetaka kufahamu sababu za serikali kutoongeza mishahara kwa wafanyakazi na kuhoji kuwa haioni kwamba inakiuka sheria ya haki za wafanyakazi.
“Serikali haioni kwamba kutopandisha mishahara wafanyakazi kunashusha ari ya kufanya kazi na kuathiri mafao ya mwisho ya wafanyakazi hao,” alihoji mbunge huyo. Waziri Mkuu alisema, baada ya kukamilisha sensa ya kuondoa wafanyakazi wasiostahili ili kuwalipa wanaostahili, utaratibu ambao ulisimamiwa na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), sasa imejikita katika kulipa madeni ya watumishi.
“Baada ya mpango huo wa kutopoteza fedha kwa kulipa wafanyakazi wasiostahili, sasa serikali imejikita katika kulipa madeni na tayari Sh bilioni 200 zimetolewa kwa ajili ya kulipa madeni hayo,” alisema.
Alisema hivi sasa nyongeza za mishahara za kila mwaka zinaendelea kutolewa, lakini kama Rais John Magufuli alivyotangaza wakati wa Mei Mosi mwaka huu Iringa, nyongeza za mishahara hazitatangazwa hadharani, kuepusha kupandisha gharama za maisha kwa wananchi.
Rais Magufuli alisema si lazima kutangaza hadharani mishahara ya wafanyakazi, kwani kufanya hivyo kunapandisha gharama za maisha ya wananchi katika kupata huduma mbalimbali.
Waziri Mkuu alisema kwa sababu mishahara ni siri ya mtu, si lazima kuitangaza hadharani, kwani kufanya hivyo kunasababisha kupanda bei na kupandisha gharama kwa wananchi kutokana na kupanda bei za vitu na huduma mbalimbali.
Majaliwa alisema lengo la serikali ni kuhakikisha inapunguza gharama kwa wananchi wake, zikiwemo za uzalishaji mali na katika masoko mbalimbali. Alitaka wafanyakazi wawe na amani na kwamba serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha maslahi yao yanazingatiwa na wakati ukifika watapata nyongeza zao. Waziri Mkuu alisema serikali imeweka utaratibu mzuri wa kuwalipa wafanyakazi stahiki.
0 Comments:
Post a Comment